Uwezo tunao, sababu tunayo, na nia tunayo
Hii ilikuwa sehemu ya hotuma ya Mwalimu J. K. Nyerere wakati akilihutubia taarifa baada ya Tanzania kuvamiwa na nduli Idd Amini Dadaa wa Uganda mwaka 1978. Kutawaliwa ni fedheha, kutawaliwa maana yake ni kupoteza uhuru na utu wako. Kwa sababu hizi za msingi Taifa la Tanzania liliingia vitani kupambana na hatimaye kumpiga nduli Idd Amin ili kuepuka fedheha na kuhakikisha uhuru wa Tanzania hauingiliwi na mtu yeyote.
Kuwa masikini maana yake ni kuwa mtumwa, kuwa masikini maana yake ni kutawaliwa, ni sawasawa na kuwa chini ya ukoloni. Mababu zetu wakiongozwa na viongozi wao akina Mkwawa, Kijekitile Ngwale, Isike, na wengine wengi walipigana kufa au kupona kupinga kutawaliwa na wakoloni kwa sababu ya fedheha waliyoipata walipokuwa wametawaliwa na wageni. Walikataa kufanyishwa kazi wasizozipenda kwa ujira mdogo ama pasipo ujira wowote, walikataa kufanyishwa kazi kwa mababu zao, walikataa kulipishwa kodi walizotozwa ili ziwasaidie watu wengine, walikataa kudhalilishwa kwa kupigwa vipoko mbele ya watoto na wake au waume zao, walikataa kupoteza heshima yao, walikataa kunyimwa haki zao za msingi kama kusafiri bila kubaguliwa, kusafiri bila vizuizi vya aina yeyote ile, kubaguliwa katika kupatiwa huduma.
Ukiwa masikini utafanyishwa kazi usizozipenda, utafanyishwa kazi kwa ujira mdogo, na utafanyishwa kazi bila ridhaa yako. Kila nikiiona mzee akifanya kazi ya fedheha kama kufagia barabara, ulinzi wakiwa na umri mkubwa naona ukoloni uletwao na umasikini, kila nikiona mtu ameshindwa kupata huduma sitahili za afya kwa sababu ameshindwa kumudu gharama za matibabu najua utumwa uletwao na umasikini ni hatari kuliko maladhi wanayougua. Kila nikiona watoto wameshindwa kupata haki yao ya msingi ya kupumuzika na kucheza kwa kufanyishwa kazi katika umri mdogo ili waweze kupata mahitaji yao, kila nikiona mtoto ameshindwa kupata haki yake ya msingi ya kupata elimu bora anayositahili naona udhalimu na mateso yaletwayo na umasikini, kila nikiona watu wakibebwa kwenye mikokoteni ama malori wakisafiri kutoka sehemu moja kwenda nyingine naona mateso yaletwayo na nduli umasikini. Kila nikiona watu wakikosa mahitaji yao ya mhimu kama malazi, chakula na mavazi wanayostahili naona umasikini ukiwa kazini, naona utumwa ule ule walioukataa mababu zetu, naona ukoloni walioukataa akina Kinjekitile, naona uvamizi alioukataa Mwalimu Nyerere.
Kinjekitile aliweza kuhamasisha majeshi ya mababu zetu kwa kutumia maji, Kinjekitile alijua tatizo kubwa lao lilikuwa liko akilini mwao; akafanikiwa kulitafutia dawa kwa kuwapa maji aliyowaaminisha kuwa yalikuwa na uwezo wa kuzuia risasi za wakoloni. Kinjekitile alifanikiwa kuwahamasisha mababu zetu na kuwatisha Wajerumani waliokuwa na siraha bora na kali zaidi kwa kutumia maji ambayo yalikuwa hayana uwezo wa kuzuia risasi kama walivyoaminishwa. Kilichowatisha Wajerumani ulikuwa ni ujasiri wa watu waliokuwa na siraha duni kuliko zao. Kilichomkimbiza nduli Idd Amin na majeshi yake ilikuwa ni ujasiri na umoja wa majeshi ya Tanzania, baada ya hotuba ile ya Nyerere kila Mtanzania alikuwa tayari kwenda vitani ingawa kila mtu alijua vita havina macho lakini walihamasika kuhakikisha kuwa taifa lao linaondokana na fedheha ya kutawaliwa. Wake kwa waume walijikusanya kumfuata, aliingiwa na hofu alivyouona umma wa Watanzania uko nyuma ya kiongozi wao wakiwa tayari kufa ili mradi wanarudisha heshima ya taifa lao.
Leo hii kuna watu wengi wamezama kwenye dimbwi la umasikini na wameridhika kuwa hawawezi kuondokana na umasikini kwa sababu hawana nyenzo, hawana siraha. Wengi, wakiwemo viongozi wa taifa letu wanadhani kuwa umasikini huo utaondolewa na watu wengine kwa kuwaonea huruma. Wengi wanajua hawawezi kuondoka kwenye bonde hilo kwa sababu ama hawana mitaji, ama hawana elimu, ama kitu kingine chochote ambacho wanadhani wakikipata wataondoka pale walipo. Historia inatuambia kuwa hili halitawezekana na halitatokea hadi pale wao wenyewe watakapokata shauri ya kuondoka kwenye kituo chao, cha umasikini na maisha duni. Ushindi wa vita yoyote huanzia akilini mwa mpiganaji, huanza pale jemedari na majeshi yake watakapoamua kuwa ni ushindi pekee ndio utawapa mapumuziko, tofauti na hapo adui atashambuliwa na kukoseshwa usingizi mpaka atakapo salimu amri. Mitaji na elimu ni vitendea kazi tu ambavyo hurahisha kazi vinapokuwepo lakini siyo sababu ya kufanikiwa.
Ndugu msomaji wangu, ni pale tu utakapo amua kuwa umasikini basi, ni pale tu utakapochukia kero na fedheha zote ziletwazo na umasikini na kuamua kuwa lazima uondokane na fedheha hizo ndipo utakoweza kuondokana na umasikini au hali duni ya maisha yako. Sitaweza, na sina uwezo wa kukueleza ni namna gani utaweza kuondoka pale ulipo kwa sababu kila mtu ana malaika wake, na kila mtu ana kipaji chake kilicho tofauti na watu wengine. Unaweza kuondokana kwa kubadilisha kazi kama utatafakali na kuona kuwa kwa namna unavyofanya si rahisi kuondokana na hali yako duni, unaweza kuendelea kufanya kazi yako ile ile lakini ukabadilisha namna unavyoifanya na namna unavyoyatumia mafao yanayotokana na kazi yako. Katika dunia hii kuna watu wamekuwa mamilionea kwa kufanya kazi unayoidharau, kuna ambao wametajirika kwa kuzoa taka, ndiyo, kuzoa taka! Kuna wengine wengi wametajirika kwa kupika, wapo pia wengi waliotajirika kwa kilimo. Kinachowatoutisha waliofanikiwa na wale ambao wameshindwa ni namna wanavyofikiri, kama ukiamua kuondokana na umasikini kwa kutumia kilimo lazima ukipende kilimo na ujiaminishe kuwa hakuna kitu kingine kitakutoa hapo isipokuwa kilimo, kama umeamua kuwa utaondokana na umasikini kwa kuokota taka lazima uzipende taka na kila unapoziona ufurahi kuwa ile ni fursa yako ya kuondokana na umasikini na siyo uchafu! Kama unataka kuondokana na umasikini ukiwa mwalimu lazima kwanza ukate shauri na kuamini kuwa ni kuwatoa watu ujinga pekee ndiko kutakako kutoa kwenye lindi la umasikini, ni lazima ufurahi kuona mtu hafahamu kitu unachokifundisha siyo kwa sababu hajui bali ni kwa sababu hiyo ni fursa yako kuondokana na umasikini, ukiwaona wanafunzi wako na mazingira ya kazi yako kuwa ni kero hautaweza hata siku moja kufanikiwa ukiwa mwalimu, ni lazima kwanza uione kazi yako kuwa ni fursa ya wewe kufanikiwa. SIRI YA USHINDI NI MOJA, KUTOPUMUZIKA HADI USHINDI UMEPATIKANA.
Tuesday, July 19, 2011
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
Nashukuru ndugu yangu Kazwile Ngwanadiyu kwa hizo post zako nzuri, Tukumbuke pia kuwa Mafanikio yanakuja vile vile kama mazingira yanapokuwa yamejengwa na jamii husika. Kama jamii imeamua kuziba mianya ya mafanikio ikaruhusu UFISADI, RUSHWA, UNYONYAJI kama ndio njia pekee za kuwatoa watu katika umasikini na kuwafanya matajiri, Mafanikio kwa watu wengi itakuwa ndoto!!! inahitaji nguvu ya ziada katika kufanikiwa. Ni sawa na mwanafunzi anasoma shule za KATA kupata Division one inawezekana kwa mtu mmoja lakini haiwezekani kwa nusu au robo ya Darasa, na lazima yule mwanafunzi awe EXTRA ORDINARY ili aweze kupata hiyo Division one. Hivyo hivyo hata kwenye mafanikio mengine ya kimaisha.
ReplyDelete